
SEHEMU A (Alama 15)
1. Soma habari ifuatayo kisha jibu maswali yanayofuata.
Ukisimama hadharani kuzungumzia suala la haki za wanaume, watu wengi watakuona mwendawazimu,
lakini wanaume wanazo changamoto kadhaa. Ni siri iliyofichuka sasa kuwa ni zamu ya wanaume
kunyanyaswa kama walivyonyanyaswa wanawake.
Kwa miongo miwili ya mwisho wa karne ya ishirini, dunia nzima imekuwa katika harakati za kutetea
haki za wanawake hususan watoto wa kike. Ni kweli kuwa mtoto wa kike amekuwa akidunishwa na
kudhulumiwa na mifumo ya kitamaduni, kisiasa na kiuchumi iliyokosa mashiko.
Wasichana walitumbukia kwenye ghilba za ndoa za mapema katika umri mdogo, hawakupata fursa ya
kwenda shule, walikeketwa na kufanyiwa dhuluma nyingine kadha wa kadha. Kutokana na hali hii, mtoto
wa kiume amekuwa akifurahia hadhi ya kuzaliwa akiwa mvulana, kwamba ndiye anayefaa zaidi ya
msichana. Si ajabu mzee mmoja kumuoza bintiye ili mahari itakayopatikana ilipe karo ya kaka yake
anayesoma. Kikao kikuu cha haki za wanawake kule Beijing China cha mwaka 1985, ni mojawapo ya
vikao vilivyomulika zaidi haki za wanawake.
Mashirika yasiyo ya kiserikali, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, serikali mbalimbali na hata makampuni
yaliunga mkono harakati za kupigana na adui mmoja "kukosekana kwa usawa wa jinsia". Lengo lilikuwa
ni kumkweza msichana ili afike alipokuwa mvulana. Misaada ikatolewa, miradi ikaanzishwa, shule
zikajengwa, mashirika ya kidini yakaibuka, mikopo ikatolewa na vyote vilimlenga huyo msichana
aliyekuwa na mahitaji makubwa ya haki. Msichana akakwea; kwa kiasi kikubwa, akakikwea kizingiti.
Hatari ya harakati hizi, ni kuelemea upande wa jinsia ya kike zaidi na kusahau wanaume. Wanaume pia
wanahitaji kupewa fursa na haki sawa kama wanawake. Tatizo la ajira kwa watoto hususan wa kiume
waishio katika mazingira magumu na hatarishi linaongezeka nchini. Visa vya wizi, uharibifu wa mali na
mauaji ya watu wasio na hatia vimezidi, aghalabu vijana ndio hutumiwa zaidi na watu wenye pesa
kufanya uhalifu huo. Wapo ambao hawaendi shule wamegeukia dawa za kulevya, wanaitwa "mateja".
Jitihada za dhati lazima zifanyike kuliokoa kundo hilo.
MASWALI
a. Andika kichwa cha habari kinachofaa kwa habari hii (maneno yasizidi matano)
b. Je, tatizo kuu linalozungumziwa katika habari uliyoisoma hapo ni lipi?
c. Taja vitendo viwili vya unyanyaswaji walivyofanyiwa wasichana kulingana na habari uliyosoma.
d. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika habari uliyosoma.
(i) Changamoto
(ii) Jinsia
(iii) Kukweza
(iv) Harakati
(v) Miongo
e. Andika ufupisho wa habari hiyo kwa maneno yasiyopungua 40 na yasiyozidi 80.