
Mtihani huu na mitihani mingine inapatikana kwenye tovuti yetu: http://maktaba.tetea.org
SEHEMU A (Alama 10)
UFAHAMU
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata:
Baba alikuwa na wajibu maalum wa kuhakikisha usalama wa familia yake. Ilimbidi awe na
nyumba watakamoishi mke na watoto. Nyumba zilijengwa kwa mitindo tofauti katika sehemu
mbalimbali hapa nchini. Wanyakyusa walikuwa na ujenzi wao ambao ni tofauti na ule wa Wahaya.
Wote wakijenga kwa ufundi wa kuvutia sana. Serikali yetu imehifadhi kwa njia ya makumbusho
nyumba zilizojengwa na wakazi wa sehemu mbalimbali hapa nchini wakitumia mitindo yao ya
asili. Nyumba hizi zipo katika kijiji cha makumbusho kilichopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Baba akishirikiana na mama walikuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa jamii yao ilipata chakula
cha kutosha. Mapema watoto nao walishiriki katika shughuli za kutafuta na kuandaa chakula.
Jamii nyingine hapa nchini zilikuwa zikishughulika na ufugaji tu. Maisha na utajiri wa jamii hizi
ulitegemea wanyama. Tangu utoto wao, mafunzo makuu yalihusu ufugaji. Kwa mfano, mtoto wa
kimasai alijifunza kuchunga na kulinda wanyama wake tangu utotoni. Ilimbidi awe askari hodari,
aweze kupambana na maadui waliotaka kuteka wanyama wao. Alitakiwa aweze kupigana na
wanyama wakali porini wenye kuishambulia mifugo. Kumuua simba ilikuwa ni ishara kubwa ya
uhodari wa kijana wa kimasai. Mafunzo ya kumwandaa kijana huyo, tangu utoto wake kwa kazi
zitakazomkabili katika maisha, yalichukua sehemu kubwa ya malezi.
Kijana wa Kihaya alikabiliwa na mazingira tofauti sana na yale mwenzie wa kimasai. Wahaya ni
wakulima, ufugaji ulichukua sehemu ndogo tu katika shughuli zao za kiuchumi. Wahaya hulima
mazao ya kudumu kama vile migomba, mashamba yao yalihitaji ulinzi na utunzaji mzuri. Hivyo
serikali imara yenye kuhakikisha amani katika nchi ili raia waweze kuendelea na kazi za kilimo
kwa amani, ilihitajika. Pia Wahaya walihitaji nyumba za kudumu; maana hali ya maisha yao
haikuruhusu uhamaji wa mara kwa mara kama vile Wamasai. Kwa hiyo mafunzo kamili
yalihitajika ili kuwaandaa watoto kwa maisha ya namna hiyo.
Maisha katika sehemu mbalimbali katika nchi yalilazimu ziwepo njia maalum za kuwalea,
kuwafundisha na kuwaandaa kwa yale yatakayowakabili katika siku za usoni.
Maswali
(a) Eleza faida mbili zinazoweza kupatikana kwa kuhifadhi mitindo ya nyumba za asili katika
kijiji cha makumbusho.
(b) Unafikiri ni sababu gani iliifanya jamii ya Kimasai kuhamahama?
(c) Kwa mujibu wa habari uliyoisoma vijana walikuwa na jukumu gani katika jamii zao?
(d) Andika kichwa cha habari kisichozidi maneno matano kinachofaa kwa habari uliyoisoma.
(e) Andika methali ya Kiswahili inayoendana na aya ya mwisho ya habari uliyoisoma.
Ukurasa wa 2 kati ya kurasa 5